26 Machi 2015 - 11:58
Wachunguzi wa ajali ya ndege wapata sauti

Wachunguzi wamepata sauti zilizorekodiwa katika moja kati ya visanduku vyeusi vinavyorekodi taarifa za safari za ndege katika ndege ya shirika la Germanwings ambayo ilianguka katika milima ya Alps

Wachunguzi  wamepata  sauti zilizorekodiwa katika  moja  kati  ya visanduku  vyeusi  vinavyorekodi  taarifa  za  safari  za  ndege katika  ndege  ya  shirika  la  Germanwings ambayo  ilianguka  katika milima  ya  Alps , na  kuuwa  watu  wote  waliokuwamo  katika  ndege hiyo.

Wachunguzi  hao  wanatarajia  kupata  taarifa  za  mwanzo  katika muda  wa  siku  kadhaa, lakini  wamesema  kazi  kubwa  zaidi itahitajika  kuweza  kutafsiri yaliyomo  katika  chombo  hicho.

 Jana  kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel  alijiunga  na  rais  wa Ufaransa  Francois Hollande  na  waziri  mkuu  wa  Uhispania Mariano Rajoy  katika  milima  ya  Alps  nchini  Ufaransa  karibu  na mahali  palipoangukia  ndege  hiyo, kukutana  na  wafanyakazi  wa uokozi  pamoja  na  wale  wa  kujitolea.

Wakati  huo  huo shirika  la  ndege  la  Ujerumani  Lufthansa limesema  haliwezi  kuthibitisha  ripoti  ya  chombo  cha  habari nchini  Marekani  juu  ya  mazingira  ambayo  yamesababisha kuanguka  kwa  ndege  ya  shirika  lake tanzu la Germanwings.

Hata  hivyo  taarifa  zinasema  mwili wa  kwanza  wa  wahanga  wa ajali  hiyo  umepatikana hii leo.

 Gazeti  la  New York  Times  limeripoti  kuwa  sauti  zinazosikika kutoka  katika  eneo  la  kuendeshea  ndege zilizonakiliwa  na kisanduku  cha  kurekodi  sauti  za  marubani  katika  ndege iliyoanguka  ya  shirika  la  Germanwings   zinaonesha  kwamba rubani  mmoja  alitoka  kutoka eneo  hilo na  hakuweza  kuingia  tena kabla  ya  ndege  hiyo  kuanguka.

Sauti  hiyo iliyorekodiwa  haikutoa  ishara  ni  kwanini  rubani aliondoka  katika  eneo  hilo na  kwanini  hakuweza  kurejea  wakati ndege  hiyo  ikielekea  taratibu  milimani siku  ya  Jumanne.

Mchunguzi  katika  ajali  hiyo  ambaye  hakutajwa  jina  amesema mtu  aliyekuwa  nje  ya  eneo  la  kuendeshea  ndege  alisikika akigonga  mlango na  hakukuwa  na  jibu.

Wakati  huo  huo  shirika la  ndege  la  Lufthansa  limetayarisha safari  kutoka  Uhispania  na  Ujerumani  kuwapeleka  ndugu  wa wahanga  wa  ajali  hiyo  katika  eneo  hilo  la  milima  ya  Alps.